Mataifa manne ya Afrika Mashariki yafuzu AFCON 2019

Hii haijawahi kutokea katika historia ya mashindano haya makubwa barani Afrika.

UMUIYA ya Afrika Mashariki (EAC) imetoa timu nne zitakazoshiriki fainali zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon 2019) zilizopangwa kufanyika Misri, Juni mwaka huu. Hii ni mara ya kwanza kwa nchi za ukanda huo kupeleka timu nne katika fainali moja ya Mataifa ya Afrika, ambazo hufanyika kila baada ya miaka miwili.

 

Timu hizo zilizofuzu ni Tanzania, Uganda, Kenya na Burundi. Tanzania inashiriki fainali hizo baada ya kucheza mara ya mwisho mwaka 1980 zilipofanyikia Lagos, Nigeria huku Burundi mwaka huu ikifuzu kwa mara ya kwanza tangu taifa hilo lipate uhuru mwaka 1962.

Timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, imefuzu kwa fainali hizo za Afcon 2019 ikishika nafasi ya pili kutoka katika Kundi L ikiwa na pointi nane, nyuma ya vinara Uganda waliomaliza wakiwa na pointi 13.

Burundi imefuzu kwa mara ya kwanza, baada ya kumaliza katika nafasi ya pili katika kundi C kwa alama 10 nyuma ya Mali.

Kenya nayo ilifuzu mechi moja kabla ya kumalizika kwa michuano ya kufuzu kutoka kundi F lililokuwa na timu tatu, baada ya Sierra Leone kufungiwa na FIFA.

Uganda nayo ilifuzu mechi moja kabla ya kumalizika kwa mechi za makundi.

Comments