Baada ya miaka 39 Tumefuzu

TIMU ya soka ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars imefuzu fainali za mataifa ya Afrika(Afcon), baada ya jana kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya  Uganda katika mchezo wa marudino uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Stars imekata tiketi hiyo iliyoisaka kwa miaka 39, baada ya kufikisha pointi nane, hivyo kuungana na Uganda iliyofuzu mapema fainali hizo, baada ya kujikusanyika pointi 13,huku ikimaliza vinara wa kundi L licha ya kipigo cha jana.

Uganda na Stars zinafanya idadi ya timu kutoka Ukanda wa Afrika Mashariki zilizofuzu fainali hizo kuwa tatu, nyingine ni Burundi.

Katika mchezo mwingine wa kundi L, wenyeji Cape Verde walilazimishwa suluhu na Lesotho jijini Praia.

Matokeo hayo yaliifanya Lesotho kufikisha pointi sita na kukamata nafasi ya tatu, huku Cape Verde ikikamata mkia baada ya kumaliza na pointi tano.

Dakika ya pili, Mbwana Samatta alishindwa kutumia vema nafasi aliyoipata kuiandikia bao la kuongoza, baada ya kupokea pasi safi ya John Bocco, ambapo aliachia mkwaju uliopaa.

Dakika ya 20, Simon Msuva aliindikia Stars bao la kuongoza, baada ya kuitendea haki pasi safi ya Bocco na kufyatua kombora lililomshinda kipa wa Uganda, Dennis Onyango.

Dakika ya 30, beki wa Stars,  Hassan Ramadhan alilimwa kadi njano, baada ya kumchezea rafu, Allan Kyambadde.

Dakika ya 45, mpira wa kichwa uliopigwa na Faruku  Miya akiunganisha krosi ya Nicholaus Wadada ilitoka nje ya lango la Stars.

Dakika 45 za kipindi cha kwanza zilikamilika , huku Stars ilitoka kifua mbele kwa bao 1-0 dhidi ya Waganda.

Kwa ujumla Stars ilitawala mchezo kipindi cha kwanza na kufanya mashambulizi mengi kwenye lango la wenyeji wao Uganda.

Stars ilitumia zaidi mipira mirefu ikianzia kwa mabeki na viungo katika kufanya mashambulizi.

Uganda  iliuanza mchezo taratibu ikionekanakusoma nyendo za Stars na kujunga mashambulizi kupitia mabeki wa pembeni  na katikati ya uwanja.

Kipindi cha pili, Stars ilirudi kwa nguvu zaidi ikilenga kupata mabao zaidi.

 

Mashambulizi ya Stars yalizaa matunda dakika ya 51, ambapo beki Erasto Nyoni aliifungia Stars bao la  pili kwa kwa mkwaju wa penalti, baada ya beki wa Uganda, Kirizestom Ntambi kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari.

Dakika ya 56, beki  Agrey Morris aliindikia Stars bao la tatu kwa kichwa akimalizia vema krosi ya Bocco.

Dakika nya 59, Kocha wa Uganda, Sebastian Desabre alifanya mabadiliko, alimtoa Emmanuel Okwi na kumwingiza Milton Karisa.

Dakika 68, Uganda ilifanya mabadiliko mengine, alitoka Faruku Miya na kuingia Lubega Edrisa kabla ya kocha Emmanuel Amunike wa Stars kufanya mabadiliko kwa kumtoa Farid Mussa na kumwingiza Himid Mao.

Ikilenga kusaka mabao, dakika ya 79, Uganda ilifanya mabadiliko, alitoka Patrick Kaddu na kuingia Shabani Muhammad kabla ya Stars kutoka John Bocco na kuingia Feisal Salumu na kisha dakika ya 89 kumtoa Simon Msuva na kumwingiza Thomas Ulimwengu.

Dakika 90 za mtanange huo zilikamilika kwa Stars kutoka uwanjani kifua mbele kwa ushindi wa mabao 3-0.

Stars ilizindua kampeni zake kwa kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Lesotho Juni 10 mwaka jana Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, kisha ikalazimisha suluhu ugenini dhidi ya Uganda.

Ikaambulia kipigo cha mabao 3-0 ugenini dhidi ya Cape Verde kabla ya kulipa kisasi nyumbani kwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0, Uwanja wa Taifa.

Baada ya kuikandamiza Cape Verde ikasafiri kwenda Lesotho ambako ilidunguliwa bao 1-0 na wenyeji.

Mara ya kwanza, Tanzania ilishiriki Afcon mwaka 1980, fainali hizo zilipofanyika nchini Nigeria.

Stars ilitinga katika michuano hiyo baada ya kuitupa nje Zambia ambayo ilikuwa inaogopwa Afrika.

Mchakato wa kufuzu wakati huo ulikuwa kwa mtindo wa mtoano, ambapo Stars ilianza kwa kumenyana na Mauritius ugenini na kukubali kichapo cha mabao 3-2, kabla ya kupindua matokeo nyumbani na kushinda mabao 3-0, hivyo kusonga mbele kwa ushindi wa jumla ya mabao 5-3.

Kutoka:  Gazeti La Mtanzania

Comments