MWALIMU wa Hisabati na Fizikia katika shule ya sekondari ya
kijiji eneo la Bonde la Ufa Kenya, Peter Tabichi (36), ameshinda Tuzo ya
Mwalimu Bora Duniani kwa mwaka 2019.
Ametwaa tuzo hiyo kati ya walimu 10,000 na kutinga 10 bora
kuwa mshindi wa dunia. Akizungumza katika hafla ya kutunukiwa tuzo yake huko
Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu, Tabichi alisema amepanga kutumia sehemu ya
fedha hizo kusaidia shule yake na jamii. Kwa kawaida, amekuwa akitoa asilimia
80 ya mshahara wake wa mwezi kusaidia masikini.
Katika hafla hiyo ya kukabidhiwa tuzo, mwenyeji wake alikuwa
nyota wa filamu kutoka Hollywood, Hugh Jackman ambapo alisema Afrika kila siku
inafungua ukurasa wa maisha. “Tuzo hii hainitambui mimi, bali inawatambua vijana
wa bara hili. Nipo hapa kwa sababu ya kile ambacho wanafunzi wangu wamefanikiwa
katika maisha yao,” alisema Tabishi na kuongeza tuzo hiyo inatoa fursa ya
ulimwengu kutambua kuwa wanaweza kufanya chochote. Alisema licha ya changamoto
za wanafunzi wake, wana juhudi kusoma kuboresha uelewa, kuibuka washindi masomo
ya sayansi Kenya.
Waandaaji wa tuzo hiyo, Taasisi ya Varkey Foundation ya
Dubai ambayo ilikuwa mara yao tano kutoa tuzo hizo za kila mwaka, wamempongeza
Tabichi kwa utendaji wake kwa kujitolea na kuaminika kwa wanafunzi wake.
Taarifa ya ushindi wa mwalimu huyo inaeleza asilimia 95 ya wanafunzi shule hiyo
wanatoka familia masikini, asilimia tatu yatima au wana mzazi mmoja wanakwenda
shule bila chakula.
“Matumizi ya dawa za kulevya, mimba za utotoni, kuanza shule
mapema, ndoa za utotoni na kujiua yanayotokea kwa wingi,” alisema. Katika shule
hizo, wanafunzi hutembea kilometa saba huku wastani wa mwalimu kwa wanafunzi ni
kila mwalimu wanafunzi 58 kukiwa na kompyuta moja na mtandao duni.
Tabichi hutumia asilimia 80 ya teknolojia na mawasiliano
kutoa mafunzo kwa wanafunzi. Rais Uhuru Kenyatta alimpongeza Tabichi kwa ujumbe
wa video na kueleza ushindi wake ni kwa Afrika. Tuzo hizo ya walimu ulimwenguni
inatolewa na taasisi ya Varkey iliyoanzishwa na Sunny Varkey, kupitia kampuni
yake ya elimu,GEMS inayoendesha shule 55 UAE, Misri na Qatar.
Kutoka : Gazeti la Habari Leo.
Comments