WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewasili jijini Cairo, Misri kwa ziara ya kikazi ya siku tatu.
Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu ameongozana na Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga na maofisa wengine wa serikali.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, katika ziara hiyo, kiongozi huyo anatarajiwa kuwa na mazungumzo na Rais wa Misri, El Sisi.
Aidha, atafanya mazungumzo na mwenyeji wake Waziri Mkuu wa Misri, Dk Moustafa Madbuoly na baadaye kukutana na wafanyabiashara wa Misri na Watanzania waishio nchini humo.
Pia Waziri Mkuu Majaliwa akiwa nchini humo, atatembelea miradi mbalimbali ya ujenzi na kilimo ili kujifunza na kuona jinsi Tanzania inavyoweza kuazima utaalamu na uzoefu.
Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa Mji mpya wa Serikali jijini Cairo, kilimo cha samaki, viwanda vya uchakataji ngozi, kituo cha kufundisha masuala ya Bahari.
Pia atatembelea mfereji wa Suez. Aidha, atashuhudia utiwaji wa saini wa mikataba mbalimbali ukiwemo mkataba wa ushirikiano wa vyombo vya habari baina ya Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) na Middle East News Agency (MENA).
Comments