Algeria dhidi ya Senegal kwenye fainali ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika 2019.

Timu hizo ambazo ziliznza mashindano katika kundi moja sawa na Tanzania na Kenya zimeibuka na ushindi dhidi ya wapinzani wao na kukata tiketi ya kuminyana tena kwenye fainali.

Kwenye hatua ya makundi, Algeria iliilaza Senegal 1-0, je matokeo hayo yatajirudia Ijumaa usiku kwenye fainali ama Senegali italipiza kisasi na kubeba kombe.

Goli la kujifunga la Tunisia katika muda wa nyongeza limewavusha Sengal mpaka hatua ya fainali ya kombe la Mataifa ya Africa (AFCON) kwa mwaka 2019.

Nusu fainali ya kwanza ilizikutanisha Senegali na Tunisia.

Japo wengi waliipigia chapuo Senegal kushinda mchezo huo, lakini ushindi haukuwa rahisi, na Tunisia 'wamekufa wakipambana'.

Dakika 90 zilitamatika bila timu yoyote kupata ushindi, huku pande zote mbili zikikosa penati katika kipindi cha pili.

Ushindi ulipatikana kwa Senegal ndani ya dakika 30 za nyongeza.

Kipa wa Tunisia Moez Hassen alifanya makosa katika dakika ya 100 kwa kuokoa vibaya mpira wa krosi na kumgonga beki wake Dylan Bronn na kuzama wavuni.

Katika dakika za mwisho za mchezo huo kukatokea 'tafrani' baada ya refa kutoa penati golini mwa Senegal kwa madai kuwa kiungo Idrissa Gana Guaye ameunawa mpira.

Hata hivyo penati hiyo ilikataliwa baada ya refa kwenda kujihakikishia kwenye mwamuzi wa msaada wa televisheni (VAR).

Hii ni mara ya pili kwa Senegal kutinga hatua ya fainali. Mara ya kwanza ikiwa 2002 ambapo walipoteza kwa mikwaju ya penati dhidi ya Cameroon.

Safari ya Tunisia kutaka kulichukua kombe hilo kwa mara ya pili imetamatika mpaka hapo yatakapofanyika mashindano mengine.

Ilipotimu nne usiku kwa saa za Afrika Mashariki, nusu fainali ya pili baina ya Algeria na Nigeria ikaanza kutimua vumbi jijini Cairo.

Nigeria ndiyo timu pekee kati ya zilizocheza nusu fainali ambayo imeshinda kombe hilo zaidi ya mara moja. Imenyakua mara tatu, mara ya mwisho ikiwa 2013.

Hata hivyo usiku wa leo, ndoto zao za kuchukua kombe hilo kwa mara ya nne zimezimwa kwa kipigo cha goli 2-1 kutoka kwa mbweha wa jangwani, Algeria.

Algeria ilitangulia kuandika goli katika dakika ya 40 ya mchezo baada ya mchezaji wa Nigeria William Troost-Ekong kujifunga.

Nigeria wakarejea mchezoni kwa goli la kusawazisha lililofungwa kupitia mkwaju wa penati na Odion Ighalo katika dakika ya 73.

Mshambuliaji hatari wa Manchester City, Riyad Mahrez ndiye aliyepeleka kilio nchini Nigeria kwa kupachika bao la ushindi kwa Algeria katika dakika ya 95.

Algeria sasa ipo mbioni kulinyakua kombe hilo kwa mara ya pili.

Mara ya kwanza na ya mwisho kwao kulinyanyua kombe hilo ilikuwa 1990, hata Mahrez ambaye ni nahodha wa kikosi cha sasa alikuwa bado hajazaliwa.

Timu tatu zenye mafanikio makubwa zaidi Afrika - Misri, Cameroon na Ghana - ziling'olewa kwenye hatua ya mtoano au maarufu kama 16 bora.

Fainali itapigwa Ijumaa katika Dimba la Kimataifa la Cairo kuanzia saa nne usiku kwa saa za Afrika Mashariki.

Japo Algeria ndiyo timu ambayo imeonesha kiwango kikubwa zaidi na ukomavu wa hali ya juu kwenye mashindano hayo mpaka sasa.

Imeshinda michezo yote - ikiwemo ushindi wa 1-0 dhidi ya Senegal - katika hatua ya makundi.

Baada ya hapo wakaitandika Guinea 3-0 kwenye hatua ya mtoano, na kisha kuwaondoa Ivory Coast kwa penati kwenye robo fainali, na leo kuwanyuka mabingwa mara tatu Nigeria kwenye nusu fainali.

Senegal ilimaliza katika nafasi ya pili kwenye kundi C na kisha kuwatoa Uganda kwenye hatua ya mtoano na kisha Benin katika hatua ya robo fainali na leo wameing'oa Tunisia kwenye nusu fainali.

Comments