Samatta kugawana zawadi na Kapombe

NAHODHA wa timu ya Taifa ya soka ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Mbwana Samatta, anayecheza katika klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji, ameliomba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kumfikiria beki wa timu hiyo, Shomari Kapombe, katika zawadi watakazopewa.

Samatta amesema hayo jana kupitia kwenye mtandao wake wa Twitter, akitaka Kapombe naye ajumuishwe kwenye mgawo wa zawadi zilizoahidiwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Stars, Paul Makonda za Sh 10,000,000 kwa kila mchezaji.

Wachezaji wa Stars, licha ya zawadi hiyo, pia waliahidiwa kiwanja kila mmoja na Rais Dk. John Magufuli kwa kufuzu michuano ya Afrika (AFCON), katika hafla ya kuwapongeza iliyofanyika juzi Ikulu, jijini Dar es Salaam, baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Uganda ‘The Cranes’.

Wengine walio katika mpango wa kupewa viwanja hivyo jijini Dodoma ni pamoja na mchezaji wa zamani wa Stars, Peter Tino, aliyeiwezesha timu hiyo kufuzu kwa AFCON mwaka 1980, mjini Lagos, Nigeria na bondia Hassan Mwakinyo, aliyemchapa bondia Sergio Gonzalez wa Argentina, katika pambano lisilo la ubingwa, lililofanyika Jumamosi, mjini Nairobi, Kenya.

Samatta katika ujumbe wake huo wa Twitter, alisema kuwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), linapaswa kumfikiria beki huyo katika zawadi zitakazotolewa na kwamba iwapo itashindikana, wachezaji wa Stars wamchangie na kama hilo litashindikana, yeye atagawana naye nusu kwa nusu katika zawadi zilizoahidiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.

“Shomari Kapombe kama Kapteni ningeomba TFF imwangalie katika zawadi ambazo wachezaji watapata, ikishindikana basi ningeomba wachezaji wote tumchangie kidogo kidogo na endapo vyote visipowezekana kabisa basi katika ahadi ya Mh Paul Makonda, nitagawana naye nusu kwa nusu,” ulisomeka ujumbe huo wa Twitter.

Wadau mbalimbali wamekuwa wakihoji hatima ya beki huyo, ambaye aliumia akiwa kwenye kikosi hicho kilichokuwa kikipigania safari ya AFCON.

 

Kapombe, ambaye ni beki wa kulia, anayechezea pia klabu ya Simba, aliumia kifundo cha mguu katika mazoezi wakati Stars ilipokuwa kambini nchini Afrika Kusini, kujiandaa na mchezo wa kufuzu kwa AFCON dhidi ya Lesotho.

Juhudi za kumpata Katibu Mkuu wa TFF, Kidao Wilfred, ziligonga mwamba kutokana na simu yake kupigiwa kwa muda mrefu bila kupokelewa.

Stars chini ya Kocha Mkuu, Mnigeria Emmanuel Amunike, ilifuzu AFCON zitakazofanyika Juni, mwaka huu nchini Misri, baada ya kufikisha pointi nane, huku Uganda ambao ni vinara wa kundi hilo wakiwa na pointi 13.

Kufuzu kwa Stars pia kumetokana na Cape Verde kutoka suluhu na Lesotho, katika mchezo uliopigwa mjini Praia.

Lesotho wamemaliza kwa kufikisha pointi sita, huku Cape Verde wakifikisha pointi tano.

Uganda ‘The Cranes’ wameungana na Stars kushiriki fainali hizo, ambapo Tanzania inatinga baada ya miaka 39, ikishiriki kwa mara ya kwanza mwaka 1980, mjini Lagos, Nigeria.

Wakati huohuo, Mwenyekiti wa Kamati ya Saidia Taifa Stars, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amesema kuwa amesikia kilio cha wachezaji wa zamani wa Stars walioiwezesha kufuzu AFCON nchini Nigeria na wameyachukua, likiwamo la Kapombe.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Makonda alitoa shukrani zake kwa wote waliofanikisha Stars kufuzu AFCON na kwamba Ijumaa itafanyika sherehe ya kuipongeza timu hiyo itakayofanyika kwenye Hoteli ya Se, Dar es Salaam.

Kutoka : Gazeti la Mtanzania

Comments